Katibu Mkuu wa UN: Ugaidi unatishia uthabiti wa bara la Afrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa ugaidi unaitishia uthabiti wa bara la Afrika.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa indhari hiyo katika ufunguzi wa mkutano wa kupiga vita ugaidi unaofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Guterres amesema, baa la ugaidi linasababisha madhara kwa familia na kuhatarisha uthabiti wa eneo lote la bara la Afrika.
Katika hotuba aliyotoa kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa siku mbili ulioanza hapo jana na kuendelea hadi leo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewafariji waathirika wa mashambulio ya kigaidi barani Afrika na kueleza kwamba, kutokana na matukio yaliyojiri karibuni kuna udharura wa Jamii ya Kimataifa kuzisaidia na kuziunga mkono nchi za Kiafrika.
Guterres amesisitiza kuwa, ugaidi usiruhusiwe kudhoofisha mwenendo wa utswai katika bara la Afrika.
Katika miaka ya karibuni, ardhi ya Kenya, hususan maeneo yake yanayopakana na Somalia imekuwa ikishuhudia mashambulio angamizi ya kigaidi, ambapo Januari 19 mwaka huu watu 21 waliuawa baada ya magaidi kushambulia hoteli moja katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, ambalo linapigana vita na serikali ya Somalia linafanya mashambulio na hujuma za kigaidi nchini Kenya na maeneo mengine ya Afrika Mashariki.
Serikali ya Kenya imekuwa ikiisaidia serikali ya Somalia katika kupambana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab kupitia kikosi cha Umoja wa Afrika AMISOM.../