Mjumbe wa AU: Pande hasimu Sudan kusaini makubaliano ya kisiasa leo
(last modified Sat, 13 Jul 2019 01:09:52 GMT )
Jul 13, 2019 01:09 UTC
  • Mjumbe wa AU: Pande hasimu Sudan kusaini makubaliano ya kisiasa leo

Wawakilishi wa Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mabadiliko wanatazamiwa kusaini makubaliano ya kisiasa leo Jumamosi, saa chache baada ya jeshi hilo kutangaza kuwa limezima jaribio la mapinduzi.

Hayo yalisemwa jana Ijumaa na Mohammed Hassan Labat, Mjumbe wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Sudan ambaye ameongeza kuwa, lengo la kusainiwa makubaliano hayo ya kisiasa ni kuondoa ombwe la uongozi na mkwamo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo tangu kupinduliwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Omar al-Bashir Aprili mwaka huu.

Naye mpatanishi wa Ethiopia katika mgogoro wa Sudan, Mahmoud Dirir amewaambia waandishi wa habari kuwa: "Tangazo hilo la kisiasa litajadiliwa na kuidhinishwa kwa wakati mmoja."

Pande mbili za Baraza la Kijeshi la Sudan na Muungano wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan, Alkhamisi ya wiki iliyopita zilifikia makubaliano maalumu ya kipindi cha mpito kwa upatanishi wa Umoja wa Afrika na Ethiopia. 

Wasudan wakishangilia baada ya pande hasimu kukubali kugawana madaraka

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka mitatu na miezi mitatu na baraza litakaloongoza nchi hiyo litakuwa na wajumbe watano wanajeshi na wajumbe watano raia. Uwenyekiti wa baraza hilo utakuwa ni wa kupokezana.

Baraza la Kijeshi la Sudan lilitwaa madaraka Aprili mwaka huu baada ya kumpindua Omar al-Bashir aliyeiongoza nchi hiyo kwa karibu miongo mitatu, kufuatia wimbi la maandamano ya wananchi.

Tags