Jul 18, 2019 12:01 UTC
  • WHO: Yumkini ugonjwa hatari wa Ebola umesambaa hadi nchini Rwanda

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mwanamke raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyeaga dunia mapema mwezi huu kutokana na homa hatari ya Ebola aliingia nchini Rwanda akiwa ameathiriwa na ugonjwa huo na huenda alisambaza virusi hivyo nchini humo kabla ya kuelekea nchini Uganda alikofia.

WHO imenukuu ripoti ya Wizara ya Afya ya Uganda inayosema kuwa, mwanamke huyo ambaye alikuwa muuza samaki alifanya safari kadhaa za kibiashara katika mji wa Goma na mji wa Gisenyi nchini Rwanda akiwa tayari ameambukizwa virusi hivyo.

Mwanamke huyo aliripotiwa kutapika mara kadhaa katika soko moja nchini Uganda mnamo Julai 11, siku chache kabla ya kuaga dunia.

Wakazi wa miji hiyo miwili ya Goma mashariki mwa Kongo DR na Gisenyi nchini Rwanda wamezitaka serikali za mataifa hayo mawili kuongeza vifaa vya uchunguzi wa homa ya Ebola mipakani.

Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Rwanda haijawahi kurekodi kesi yoyote ya ugonjwa wa Ebola.

Mkazi wa Goma, DRC akipewa chanjo ya Ebola

Mwezi uliopita, watu watatu waliaga dunia wilayani Kasese, mashariki mwa Uganda kutokana na mlipuko wa Ebola uliongia nchini humo ukitokea nchini jirani ya DRC.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu zaidi ya 1,700 wameaga dunia ndani ya miezi 11 iliyopita kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola tangu uripuke upya nchini Kongo DR mwezi Agosti mwaka jana 2018.

Tags