Makumi ya magaidi waangamizwa na jeshi la Misri eneo la Sinai
Jeshi la Misri limetangaza kuwa limeua magaidi 20 katika operesheni ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini.
Taarifa ya jeshi hilo imesema magaidi hao waliuawa jana Ijumaa katika shambulizi la anga la vikosi vya serikali dhidi ya maficho ya magaidi hao katika miji ya al-Arish na Bir al-Abd katika Peninsula ya Sinai.
Jeshi hilo limesema lilizishambulia ngome 100 za magaidi hao katika operesheni hiyo ya jana.
Operesheni ya jana ya vikosi vya usalama vya Misri imefanyika siku moja baada ya raia mmoja na mwanajeshi mmoja kuuawa katika shambulizi la bomu lililotekelezwa na magaidi katika mji wa Sheikh Zuweid, eneo la Sinai Kaskazini.
Mapema mwezi huu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ilitangaza habari ya kuuawa askari wanane wa serikali katika shambulizi la magaidi kwenye mji wa al Arish katika mkoa wa Sinai wa kaskazini mwa nchi hiyo. Aidha magaidi watano waliuawa katika mapigano hayo.
Mapigano huwa yanatokea mara kwa mara baina ya magenge ya kigaidi na jeshi la Misri katika mkoa wa Sinai ulioko kaskazini mwa nchi hiyo na katika baadhi ya maeneo mengine ya Misri.