Aug 01, 2019 12:48 UTC
  • Mpaka wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
    Mpaka wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Serikali ya Rwanda imefunga mpaka wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya kugunduliwa kesi ya tatu ya muathirika wa virusi vya ugonjwa wa Ebola katika mji wa mpakani wa Goma.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya maafisa wa serikali ya Congo kuthibitisha kuwa binti wa mgonjwa wa Ebola katika mji huo wa Goma ameambukizwa ugonjwa huo. Hilo ni tukio la tatu la maambukizi ya virusi vya Ebola katika mji huo ulioko kwenye mpaka wa Congo na Rwanda wenye jamii ya wakazi wasiopungua milioni moja.

Waziri wa Nchi katika Masuala ya Kigeni wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe amewaambia waandishi habari kwamba, mpaka wa nchi hizo mbili umefungwa lakini hakutoa maelezo zaidi.

Ripoti ya kugunduliwa kesi zaidi za maambukizi ya Ebola katika mji wa Goma inazidisha wasiwasi wa kueneza zaidi ugonjwa huo kwenye eneo hilo lenye idadi kubwa ya watu ambalo liko umbali wa kilomita zaidi ya 350 kutoka mahaka ugonjwa huo ulipogundulika kwa mara ya kwanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ugonjwa wa Ebola umeua mamia ya watu Congo DR 

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu zaidi ya 1,700 wameaga dunia ndani ya miezi 11 iliyopita kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola tangu uripuke upya nchini Kongo DR mwezi Agosti mwaka jana 2018.

Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa Afrika.

Tags