Mgombea urais wa Jumapili ya kesho Tunisia aendelea kushikiliwa mahabusu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55987-mgombea_urais_wa_jumapili_ya_kesho_tunisia_aendelea_kushikiliwa_mahabusu
Mahakama ya Rufaa ya Tunisia imekataa ombi la mgombea urais katika kinyang'anyiro cha Jumapili ya kesho, Nabil Karoui la kuachiwa huru kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 13, 2019 22:37 UTC
  •  Mgombea urais wa Jumapili ya kesho Tunisia aendelea kushikiliwa mahabusu

Mahakama ya Rufaa ya Tunisia imekataa ombi la mgombea urais katika kinyang'anyiro cha Jumapili ya kesho, Nabil Karoui la kuachiwa huru kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Kamel Ben Massoud ambaye ni wakili wa Nabil Karoui amesema kuwa, mteja wake atabakia mahabusu anakoshikiliwa kwa tuhuma za kukwepa kulipa kodi na utakatishaji wa fedha chafu.

Nabil Karoui ambaye ni miongoni mwa wagombea 26 wa uchaguzi wa rais nchini Tunisia amekanusha madai hayo akisema kesi hiyo imechochewa na malengo ya kisiasa.

Wafuasi wa tajiri na mliliki huyo wa vyombo vya habari wanawatuhumu wapinzani wake wenye nguvu na madaraka kwamba wanajaribu kumnyamazisha na kusitisha kampeni yake inayokosoa sera za serikali na hali mbaya ya uchumi.

Wapinzani wa Karoui wanamtuhumu kwamba, ametumia kituo chake cha runinga ambacho hakijaidhinishwa na michango anayokusanya kwa maslahi yake binafsi ya kisiasa.

Uchaguzi wa rais wa Tunisia umepangwa kufanyika Jumapili ya kesho ukiwashirikisha wagombea 26.

Watunisia laki nne waliojiandikisha kupiga kura nje ya nchi walishiriki katika zoezi hilo lililoanza jana katika nchi za kigeni.  

Huu ni uchaguzi wa pili wa kidemokrasia kufanyika nchini Tunisia tangu baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El-Abidine Ben Ali mwaka 2011.

Watunisia wakichoma picha ya Ben Ali

Ben Ali aliitawala kidikteta Tunisia bila upinzani kwa muda wa miaka 23, lakini alilazimishwa kung'atuka madarakani kutokana na vuguvugu la umma lililochochewa na kifo cha kijana mmoja msomi aliyelazimika kuwa muza mboga, ambaye aliamua kujichoma moto baada ya kunyang'anywa bidhaa zake na polisi.

Ripoti zinasema dikteta huyo wa zamani wa Tunisia amelazwa hospitalini alikokimbilia nchini Saudi Arabia na hali yake kiafya inaripotiwa kuwa ni mbaya sana.

Uchaguzi wa kesho nchini Tunisia unafanyika kufuatia kifo cha rais wa nchi hiyo, Beji Caid Essebsi, kilichotokea mwezi Julai mwaka huu.