Ushindi wa mgombea wa kujitegemea katika uchaguzi wa Rais nchini Tunisia
Duru ya pili ya uchaguzi wa Rais nchini Tunisia ilifanyika jana Jumapili na matokeo yasiyo rasmi yanaonyesha kuwa, mgombea wa kujitegemea Kais Saied ameibuka na ushindi kwa kujipatia asilimia 75 ya kura.
Duru ya pili ya uchaguzi huo iliwashirikisha mgombea wa kujitegemea Kais Saied na Nabil Karoui wa chama cha Qalb Tunes. Matokeo ya awali ya duru ya pili ya uchaguzi wa Rais wa Tunisia yanaonyesha kuwa Kais Saied amepata asilimia 75 ya kura na Nabil Karoui pia ameambulia karibu asilimia 24 ya kura. Tume ya Uchaguzi ya Tunisia ilitarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya duru ya pili ya uchaguzi huo leo Jumatatu.
Kwa muktadha huo, Kais Saied anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa Rais mpya wa Tunisia na kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Kais ameibuka na ushindi katika hali ambayo, alikataa kujiunga na mrengo na chama chochote cha kisiasa katika kampeni za uchaguzi na hata alikataa kupokea ruzuku ya serikali inayotolewa kwa wagombea. Pamoja na hayo, Kais Saied alipata himaya na uungaji mkono wa Chama cha Kiislamu cha al-Nahdha ambacho kimeibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge.
Emad al-Khamiri msemaji wa Chama cha al-Nahdha alitangaza kabla ya uchaguzi wa jana kuwa, wanawataka wafuasi wao wote wampigie kura Kais Saied katika uchaguzi wa Rais.
Kais Saied ni mwanasheria mstaafu ambaye amekuwa akisisitiza juu ya vyombo vya mahakama kufanya kazi zake kwa uhuru pasina ya kuingiliwa na udharura wa kutekelezwa sheria kwa wote. Aidha moja ya mambo aliyokuwa akisisitiza kwamba, atayapa kipaumbele endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tunisia ni kupambana na ufisadi ambao anasema umechangia kushadidi umasikini na ukosefu wa uadilifu wa kiijamii katika nchi hiyo. Ufisadi ni miongoni mwa matatizo makuu hivi sasa nchini Tunisia kiasi kwamba, weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, ufisadi nchini humo ulishadidi zaidi baada ya Januari 14 mwaka 2011, siku ambayo mapinduzi ya umma yalipata ushindi.
Njama za baadhi ya madola ya Kiarabu ya kieneo za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya Tunisia ni jambo jingine ambalo limezusha wasiwasi mkubwa katika nchi hiyo kiasi kwamba, Hamadi al-Jebali, Waziri Mkuu wa zamani wa Tunisia amesema kuwa, Imarati imekuwa ikikiuka mamlaka ya kujitawala Tunisia kutokana na kutwisha matakwa yake na kutumia vyombo vya habari dhidi ya Tunis.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi wa Rais, Kais Saied sambamba na kusisitiza kuwa, mipango yake imejengeka juu ya kuheshimu uhuru amesema kuwa, kipindi cha Tunisia kuwa chini ya usimamizi wa nchi nyingine kimefikia tamati. Rais mteule wa Tunisia amezungumzia pia sera zake za kigeni na kueleza kwamba, analipa kipaumbele suala la Palestina na kwamba, kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ni khiyana na usaliti mkubwa.
Aidha akihutubia baada ya kushinda kiti cha Urais nchini Tunisia, Kais Saied amesisitiza kuwa, anaunga mkono masuala ya uadilifu kubwa zaidi ikiwa kadhia ya Palestina na kwamba, kuna haja ya kuweko kipengee katika katiba ya Tunisia kinachotambua kuwa ni uhalifu kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel.
Tunisia ni nchi pekee ya Kiarabu ambayo baada ya mapinduzi ya umma ya mwaka 2011 ilibadilika kutoka katika mfumo wa chama kimoja chenye kuhodhi kila kitu na kuwa na mfumo wa kisiasa wa kidemokrasia. Hivi sasa inaonekana kuwa, nchini Tunisia kumeanza maisha mapya ya kisiasa hasa kutokana na Chama cha al-Nahdha kilichopata viti vingi vya Bunge kuwa pamoja na Rais mteule, jambo ambalo linaweza kuwa hatua muhimu ya kuifanya demokrasia ichukue mkondo wake katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kwa sasa tunapasa kusubiri na kuona matukio ya baada ya uchaguzi nchini Tunisia yatakuwa na taathira gani kwa hali ya ndani na siasa za kigeni za nchi hiyo hususan kuhusiana na Palestina na masuala yanayohusiana na kadhia hiyo.