Wito watolewa kuwachukulia hatua waliotenda jinai Jamhuri ya Afrika ya Kati
Jumuiya za kutetea haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati zimetoa wito wa kuchukuliwa hatua za kisheria wale wote waliohusika na jinai na vitendo vya utumiaji mabavu nchini humo.
Watetezi wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekusanya mlolongo wa saini na kumtaka Rais mpya wa nchi hiyo Faustine Archange Touadera kulipa kipaumbele katika serikali yake suala la kutiwa mbaroni na kupandishwa kizimbani watu waliohusika na jinai na machafuko nchini humo.
Bruno Gbie-Gba, ambaye ni mjumbe wa asasi iitwayo Muungano wa Afrika ya Kati Kwa Ajili ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai amesema kuwa, nchi hiyo imo katika hali ya kukivuka kipindi cha mgogoro lakini pamoja na hayo waathirika wa mgogoro huo hawapasi kusahauliwa.
Mwanaharakati huyo wa masuala ya haki za binadamu amesema, serikali mpya chini ya uongozi wa Rais Faustine Archange Touadera inapaswa kuzihakikishia familia za waathirika wa machafuko ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba, jinai na vitendo vya mauaji na utumiaji mabavu vilivyofanywa nchini humo havitabakia hivi hivi bila ya wahusika kupandishwa kizimbani.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko na mapigano tangu mwaka 2013 wakati makundi ya Kikristo yanayobeba silaha yalipoanzisha mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya kundi la Seleka lenye Waislamu wengi zaidi, ambalo mnamo mwezi Machi mwaka huo liliiondoa madarakani serikali ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Francois Bozize.