Imarati yatuhumiwa kuhusika na shambulizi la anga lililoua wahajiri 53 Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57104-imarati_yatuhumiwa_kuhusika_na_shambulizi_la_anga_lililoua_wahajiri_53_libya
Nyaraka za siri za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, ndege ya kivita ya nchi ajinabi ndiyo iliyotekeleza shambulizi la anga lililolenga kituo cha kuwazuilia wahajiri haramu mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuua makumi miongoni mwao.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Nov 06, 2019 21:43 UTC
  • Imarati yatuhumiwa kuhusika na shambulizi la anga lililoua wahajiri 53 Libya

Nyaraka za siri za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, ndege ya kivita ya nchi ajinabi ndiyo iliyotekeleza shambulizi la anga lililolenga kituo cha kuwazuilia wahajiri haramu mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuua makumi miongoni mwao.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa bila kutaja jina la nchi yoyote, wanasema kuwa hujuma hiyo ya mwezi Julai mwaka huu ilitekelezwa na ndege ya kijeshi ya nchi ya nje kwa niaba ya kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar.

Duru zilizo karibu na uchunguzi huo wa UN hata hivyo zimeashiria kuwa, yumkini ndege iliyotekeleza shambulizi hilo ni ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Imarati haijato tamko lolote kuhusiana na madai hayo.

Shambulio hilo la anga la Julai 2 katika mji wa Tajoura, viungani mwa Tripoli liliua wahajiri wa Kiafrika wapatao 53 na kujeruhi wengine 130. Umoja wa Mataifa ulitaja shambulio hilo kama jinai ya kivita.

Drone ya Imarati iliyotunguliwa nchini Libya

Kundi hilo la Khalifa Haftar, kwa msaada na uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi, tarehe 4 Aprili mwaka huu lilianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli, hatua ambayo imelaaniwa na jamii ya kimataifa.

Tangu vikosi hivyo vya Haftar vilipoanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu huo wa Libya hadi sasa, zaidi ya watu 1,090 wameuawa na wengine wasiopungua 5,700 wamejeruhiwa.