UN: Imarati, Sudan na Jordan ziliwapa wapiganaji wa Haftar silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57172-un_imarati_sudan_na_jordan_ziliwapa_wapiganaji_wa_haftar_silaha
Rasimu ya ripoti ya Umoja wa Mataifa imefichua kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sudan na Jordan zimekiuka vikwazo vya silaha vya umoja huo kwa kulipa silaha kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2019 04:01 UTC
  • UN: Imarati, Sudan na Jordan ziliwapa wapiganaji wa Haftar silaha

Rasimu ya ripoti ya Umoja wa Mataifa imefichua kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sudan na Jordan zimekiuka vikwazo vya silaha vya umoja huo kwa kulipa silaha kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Jopo la Wataalamu wa Kamati ya Kimataifa ya Vikwazo Dhidi ya Libya imesema kuwa, Jeshi la Sudan chini ya Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hameti) lilikiuka azimio la Umoja wa Mataifa kwa kutuma wanajeshi wake wapatao 1000 mashariki mwa Libya mwezi Julai mwaka huu, kwa ajili ya kuwaunga mkono wapiganaji wa Haftar.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Imarati na Jordan zinatuhumiwa kulipa silaha kundi hilo la Haftar, huku Uturuki ikidaiwa kuipa uungaji mkono wa silaha Serikali ya Mapatano ya Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, inayotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa.

Siku chache zilizopita, nyaraka za siri za Umoja wa Mataifa zilifichua kuwa, ndege ya kivita ya nchi ajinabi ndiyo iliyotekeleza shambulizi la anga lililolenga kituo cha kuwazuilia wahajiri haramu mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli na kuua makumi miongoni mwao. Duru zilizo karibu na uchunguzi huo wa UN zimeashiria kuwa, yumkini ndege iliyotekeleza shambulizi hilo la Julai 2 katika mji wa Tajoura, viungani mwa Tripoli lililoua wahajiri wa Kiafrika wapatao 53 na kujeruhi wengine 130 ni ya Umoja wa Falme za Kiarabu.

Jenerali Haftar (kushoto) alianzisha vita siku chache baada ya kukutana na Mfalme Salman wa Saudia, mjini Riyadh

Kundi hilo la Khalifa Haftar, kwa msaada na uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi, tarehe 4 Aprili mwaka huu lilianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli, hatua ambayo imeendelea kulaaniwa na jamii ya kimataifa.

Tangu vikosi hivyo vya Haftar vilipoanzisha hujuma na mashambulio dhidi ya mji mkuu huo wa Libya hadi sasa, zaidi ya watu 1,090 wameuawa na wengine wasiopungua 5,700 wamejeruhiwa.