UNFPA yataka dhuluma dhidi ya wanawake katika jamii zikomeshwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57268-unfpa_yataka_dhuluma_dhidi_ya_wanawake_katika_jamii_zikomeshwe
Mmoja kati ya wanawake watatu duniani hukumbana na dhuluma za kijinsia kutoka kwa wapenzi au waume zao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 14, 2019 10:58 UTC
  • UNFPA yataka dhuluma dhidi ya wanawake katika jamii zikomeshwe

Mmoja kati ya wanawake watatu duniani hukumbana na dhuluma za kijinsia kutoka kwa wapenzi au waume zao.

Haya yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), Dkt Natalia Kanem, katika Kongamano la Kimataifa Kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD) linalofanyika mjini Nairobi. Amesema unyama huo sasa unachukuliwa kuwa jambo la kawaida.

Kwenye kongamno hilo linalotarajiwa kumalizika leo katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa KICC, wajumbe walichukua muda kuwakumbuka wahanga wa dhulma za kijinsia. Ilifichuliwa zaidi kwamba kila siku, wanawake na wasichana 137 huuawa na jamaa zao.

Kuhusiana na takwimu hizo, Dkt Kanem alisema kwamba haitakuwa haki ikiwa jamii ya kimataifa itaendelea kukaa kimya huku wanawake wakiendelea kudhulumiwa.

“Ndiposa tunashirikiana na mradi wa Spotlight Initiative ili kukabiliana na aina zote za dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana,” ameema Dkt Kanem.

Pia akizungumza kwenye kikao hicho, Bi Gita Sen, profesa wa hazina ya afya ya umma nchini India, alisema kwamba 58% ya dhuluma dhidi ya wanawake hutekelezwa na wapenzi, waume au jamaa zao.

Dhulma dhidi ya wanawake

Amesema kuwa "Hii ni ina maana kwamba nyumbani ndio sehemu hatari zaidi kwa mwanamke.”

Bi Phumzile Mlambo- Ngucka, Mkuregenzi Mtendaji wa UN Women amesema katika kongamano la Nairobi kwamba kunyimwa uwezo wa kiuchumi kumewafanya wanawake wawategemee sana wanaume, suala linalowaweka katika hatari zaidi ya kukumbana na dhuluma.

Kuligana na Bi Mlambo, serikali zinapaswa kuhakikisha suala la kuwepo kwa taasisi za kuwapigania na kuwalinda wanawake dhidi ya dhuluma za kijinsia.