Jubaland: Majeshi ya Ethiopia na Somalia yanataka kumpindua Rais Madobe
Serikali ya eneo lenye mamlaka ya ndani la Jubaland, Kusini mwa Somalia imedai kuwa wanajeshi wa Ethiopia wanakula njama za kumpindua Rais Ahmed Madobe wa jimbo hilo.
Jubaland imemuandikia barua James Swan, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, ikimtaka aingilie kati na kulizuia jeshi la Ethiopia kuingilia mambo ya ndani ya eneo hilo.
Katika barua hiyo, serikali ya Jubaland imedai kuwa, jeshi la Ethiopia linapanga njama za chini kwa chini na Serikali ya Federali ya Somalia za kuanzisha vuguvugu la mapinduzi yatakayomuondoa madarakani Rais Madobe na pia kusambaratisha operesheni za kiusalama katika mji bandari wa Kismayo.
Sheikh Ahmed Madobe alihifadhi kiti chake baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa urais uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Jubaland imesema Ethiopia ambayo ina maelfu ya wanajeshi nchini Somalia ikiwa ni sehemu ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, imetuma wanajeshi ambao sio wanachama wa vikosi hivyo vya AU katika eneo la Gedo kinyume cha sheria, na kwa kushirikiana na serikali ya Mogadishu wamevuruga umoja, usalama na uthabiti wa kisiasa katika eneo hilo la kaskazini mwa Jubaland.
Mfumo wa utawala Somalia ni wa kifiderali ambapo majimbo kadhaa nchini humo yana mamlaka ya ndani ya kujitawala.