Ripoti ya Independent: Kengele za vita zasikika zaidi katika milango ya Libya
Ripoti iliyotolewa na gazeti la Independent la Uingereza imefichua kuwa, mapatano tete ya kusitisha vita yaliyofikiwa hivi karibuni baina ya madola makubwa mjini Berlin huko Ujerumani yanaelekea kuporomoka kutokana na mashambulizi ya anga yanayoshuhudiwa sasa nchini Libya na vitisho vinavyoendelea kutolewa na pande hasimu.
Ripoti hiyo inasema kuwa, jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi kimataifa limetangaza kuwa, limetungua ndege ya kijeshi isiyo na rubani inayoaminika kuwa ilikuwa ikitumiwa na Imarati. Ndege hiyo imetungliwa baada ya Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kupata silaha mpya za kutungua ndege zilizoingizwa nchini humo na majeshi ya Uturuki.
Ripoti hiyo pia imeashiria kushadidi kwa mapigano kandokando ya mji wa Tripoli na karibu na mji wa tatu kwa ukubwa nchini Libya wa Misrata baada ya utulivu wa kiasi fulani uliopaikana kufuatia mkutano wa tarehe 12 mwezi huu wa Februari huko Russia na kusema kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka mapigano hayo hususan baada ya Umoja wa Mataifa kutahadharisha kuwa pande mbili zinazozozana zimendelea kupokea ndege zilizosheheni aina mbalimbali na silaha za zana za kisasa za vita licha ya marufuku ya kutuma silaha nchini Libya iliyotangazwa katika mkutano wa wiki kadhaa mjini Berlin.
Ripoti ya gazeti la Independent imesema kuwa, Uturuki inayoisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inatuma silaha kwa muitifaki wake na kuwapelekea wapiganaji wa makundi ya kigaidi ya Syria nchini Libya huku Imarati ikiendelea kumimina matani ya silaha kwa jeshi linaloonozwa na Jenerali mstaafu, Khalifa Haftar.
Libya ilitumbukia katika vita na machafuko ya ndani yaliyochochewa na nchi za kigeni baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Mgogoro wa Libya umezidi kuwa mkubwa baada ya jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati na Misri kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli mwezi Aprili mwaka jana.