Waziri Mkuu wa Sudan aghadhabishwa na mkutano wa Burhan na Netanyahu
Waziri Mkuu wa Sudan amekosoa vikali mkutano wa Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel.
Abdalla Hamdok alisema hayo jana Jumatano na kusisitiza kuwa, uamuzi wowote kuhusu masuala ya nje ya Sudan unapaswa kuchukuliwa na Baraza la Mawaziri la nchi hiyo na wala sio mtu binafsi.
Waziri Mkuu huyo amesema serikali ya Sudan anayoiongoza haikushauriwa chochote kuhusiana na mkutano huo wa siri na kwamba wamekuja kulifahamu suala hilo baadaye kupitia vyombo vya habari.
Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, Hamdok amesema, "barabara ya kuelekea katika mabadiliko ya maana nchini Sudan imezingirwa na changamoto na vizingiti vingi."
Matamshi hayo ya Waziri Mkuu wa Sudan ni katika mlolongo wa kauli za kokosolewa vikali kitendo cha Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kukutana na kufanya mazungumzo na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Uganda.
Siku ya Jumanne, chama cha upinzani cha Congress ya Wananchi cha Sudan kililaani vikali mkutano huo wa kificho, kikisisitiza kuwa unaenda kinyume na msimamo wa watu wa Sudan wa kuwaunga mkono Wapalestina katika mapambano yao dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.
Mkutano huo wa Jumatatu baina ya Jenerali al-Burhan na Netanyahu nchini Uganda umelalamikiwa vikali ndani na nje ya Sudan, ambapo siku ya Jumanne wananchi wa Sudan waliokuwa na hasira waliandamana mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu mjini Khartoum kuulaani.