50 wauawa katika shambulio la watu waliobeba silaha Nigeria
Watu wasiopungua 50 wameuawa baada ya genge la watu waliobeba silaha kushambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa Nigeria.
Gavana wa jimbo hilo, Nasiru El-rufai amesema wahalifu waliotekeleza ukatili huo siku ya Jumapili wanatoka katika majimbo jirani ya Katsina na Zamfara na pia Jamhuri ya Niger. Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mauaji hayo jimboni Kaduna.
Naye msemaji wa polisi nchini Nigeria, Muhammed Jalige amethibitisha habari ya kutokea mauaji hayo, ambapo amesema vijiji vilivyoshambuliwa katika hujuma hiyo iliyofanyika kuanzia saa kumi na moja jioni hadi saa mbili usiku wa kuamkia jana ni Hashimawa, Marina, Kerawa, Unguwan Musa na Zariyawa.
Nchi ya Nigeria imeendelea kushuhudia machafuko hasa maeneo ya kaskazini na mashariki mwa nchi hiyo kutokana na kuweko harakati za waasi na kundi la kigaidi la Boko Haram.
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake katika nchi jirani pia za Niger, Chad na Cameroon.
Kuanzia wakati huo hadi sasa, zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao.