Waziri Mkuu wa Sudan anusurika kifo katika shambulio la bomu
(last modified Mon, 09 Mar 2020 10:15:34 GMT )
Mar 09, 2020 10:15 UTC
  • Waziri Mkuu wa Sudan anusurika kifo katika shambulio la bomu

Waziri Mkuu wa Sudan Abdulla Hamdok amenusurika kifo leo kufuatia mlipuko wa gari uliolenga gari lake katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.

Mke wa Waziri Mkuu wa Sudan amenukuliwa akisema kuwa, mume wake leo amenusurika kifo katika shambulio la bomu lililolenga kumuua na kwamba, baada ya tukio hilo amehamishiwa katika sehemu salama.

Baadhi ya duru zimeonyesha magari kadhaa yaliyoegeshwa yakiwa yameharibiwa vibaya baada ya mlipuko unaosadikiwa kuwa ulikusudia kumuua Waziri Mkuu wa Sudan.

Taarifa za awali zinasema kuwa, mlipuko huo ulilenga magari mawili ambapo moja lilikuwa limembeba Waziri Mkuu huyo wa Sudan. Ripoti zinaeleza kuwa, Abdullah Hamdouk hakupata majeraha yoyote katika shambulio hilo la bomu ingawa mmoja wa walinzi wake amejeruhiwa katika tukio hilo.

Inaelezwa kuwa, mlipuko huo umetokea jirani na gereza la Kobar anamotumikia kifungo aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Omar Hassan al-Bashir.

Omar al-Bashir Rais wa zamani wa Sudan ambaye kwa sasa anatumikia kifungo jela

Abdulla Hamdok aliteuliwa kuchukua wadhifa wa Waziri Mkuu wa Sudan Agosti mwaka jana baada ya maandamano makubwa yaliyomuondoa madarakani Omar al-Bashir na kisha jeshi kuchukua utawala wa nchi ambalo nalo lililazimika kukabidhi madaraka kwa utawala wa raia.

Sudan ilianza kushuhudia wimbi la maandamano ya wananchi kuanzia katikati ya mwezi Disemba mwaka jana dhidi ya hali mbaya ya uchumi; na kufuatia ghasia hizo jeshi la Sudan tarehe 11 Aprili mwaka huu lilimpindua madarakani rais huyo wa zamani na kushika hatamu za uongozi kwa kuunda baraza la kijeshi.