AU yalaani ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani vikali mauaji ya raia mweusi nchini Marekani katika jimbo la Minnesota, licha ya kuwa hakuwa na silaha yoyote.
Moussa Faki Mahamat amelaani ukiukwaji wa haki wa maafisa wa jeshi la Polisi mjini Minneapolis na kitendo kilichopelekea kuuawa kwa mmarekani mweusi.
Musa Faki ametoa salamu za rambi rambi kwa familia ya George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuawa kwa kukandamizwa na goti shingoni na askari mweupe.
Kiongozi huyo wa AU amekumbusha kuwa, tangu kuasisi kwa umoja huo mwaka 1964, umekuwa ukilaani vitendo vya ubaguzi wa rangi. Amesema viongozi wa Marekani wanatakiwa kuongeza juhudi za kukomesha ubaguzi wa rangi nchini humo.
Kadhalika Kwesi Quartey, Naibu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani mauaji hayo na kusema: "Kifo kingine cha Marekani-Mweusi, kwa sababu ya kuwa mweusi. Huenda sisi ni weusi, lakini sisi ni wanadamu pia."
Kufuatia kushtadi maandamano na ghasia katika kona mbali mbali za Marekani kufuatia ukatili huo, afisa wa polisi aliyetekeleza jinai hiyo ameshtakiwa kwa kosa la mauaji. Derek Chauvin, afisa wa polisi mzungu ambae video yake ya kutekeleza ukatili huo imesambaa katika mitandao ya kijamii, anakabiliwa na mashitaka ya mauaji, kusababisha kifo pasipo kukusudia na mauaji kwa kizembe.