Independent: Wafanyabiashara wa Kimagharibi wamemtapeli Haftar mamilioni ya dola
Gazeti la Independent linalochapishwa nchini Uingereza limefuchua kwamba mamluki wa nchi za kigeni na wafanyabiashara wa nchi za Magharibi wakiwemo Waingereza, wamemtapeli jenerali muasi Khalifa Haftar mamilioni ya dola za Kimarekani.
Independent limefichua kuwa, Haftar alitoa fedha hizo mkabala wa kupewa silaha na huduma za kijeshi lakini hakupewa silaha wala huduma hizo za kijeshi.
Gazeti hilo ambalo limenukuu duru za kidiplomasia na watu waliohusika katika muamala mwingine kama huo, limeripoti kuwa, kipigo alichopata jenerali Haftar katika medani za kijeshi mbele ya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kifaifa siyo sababu pekee ya hasara kubwa ya fedha ya kundi hilo linalopigana dhidi ya serikali inayotambuliwa rasmi kimataifa ya Libya.
Ripoti hiyo imefichua kuwa Haftar ametapeliwa zaidi ya dola milioni 55 zilizotolewa kwa ajili ya manunuzi ya zana za kivita zikiwemo ndege za upelelezi lakini hakupewa zana hizo.
Ripoti hiyo imesema kuwa, Jenerali Haftar ambaye aliwalipa mamluki na wafanyabiashara hao wa Kimagharibi dola milioni 80 hakupewa isipokuwa helikopta sita zilizochakaa ambazo wataalamu wanasema thamani yake haizidi dola milioni 14.
Baina ya mwaka 2016 na 2017 pia Haftar alimlipa mfanyabiashara mmoja wa Marekani dola milioni 6.5 kwa ajili ya manunuzi ya meli ya doria habarini lakini Mmarekani huyo alitoweka na fedha bila ya kukabidhi mzigo huo.
Katika wiki za hivi karibuni kundi la Khalifa Haftar limelazimika kuondoka katika maeneo mengi ya kistratijia ya Libya baada ya vipigo mtawala mkabala wa jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kiaifa.
Kundi la Khalifa Haftar linaungwa mkono na kusaidiwa na nchi kama Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi hasa Ufaransa.