UN yabainisha wasiwasi wake kuhusu uingiliaji wa nchi ajinabi huko Libya
Mjumbe wa muda wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amekosoa uingiliaji wa madola ajinabi nchini humo.
Bi Stephanie Williams amekosoa uingiliaji wa nchi ajinabi katika masuala ya Libya na kueleza kuwa raia wa nchi hiyo wana wasiwasi kuhusu mustakbali wao. Bi Williams amesisitiza namna watu wa Libya walivyochoka na vita na wanataka amani na kuongeza kuwa: Walibya wanataka kusitishwa mapigano nchini mwao.
Libya ilitumbukia katika mapigano na mgogoro wa kisiasa mwaka 2011 baada ya Marekani na nchi wanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuingilia kati malalamiko ya wananchi na kumuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.
Kwa sasa nchi hiyo ina serikali mbili; moja ikiwa ile inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa yenye makao makuu huko Tripoli, mji mkuu wa Libya chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Fayez al Sarraj, na serikali yenye makao makuu katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi inayosaidiwa na Imarati, Misri, Saudi Arabia na nchi kadhaa za Ulaya.