IGAD yafurahishwa na makubaliano ya amani ya Sudan
Jumuiya ya Maendeleo ya Serikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD imepongeza makubaliano yaliofikiwa hivi karibuni baina ya Serikali ya Sudan na Muungano wa Harakati ya Kimapinduzi kutoka jimbo la Darfur na katika majimbo ya kaskazini ili kuhitimisha mgogoro wa miaka 17 nchini humo.
IGAD imesema ni jambo la kupongezwa na kutia matumaini kwa pande hizo kusaini makubaliano hayo ya amani kwa ajili ya mustakabali wa wananchi wote wa Sudan.
Taarifa ya jumuiya hiyo ya kikanda imesema: Ni matumaini yetu kuwa pande ambazo hazijasaini makubaliano hayo, karibuni yataungana na ndugu zao katika jitihada hizo za kuhitimisha matatizo yanayowakabili Wasudan.
Hafla rasmi ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilifanyika juzi huko Juba mji mkuu wa Sudan Kusini. Juba imekuwa ikijishughulisha kama mwenyeji na kusaidia jitihada za upatanishi katika mazungumzo yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu ya Sudan tangu mwishoni mwaka 2019.
Pamoja na hayo, makundi mawili ya waasi yamepinga makubaliano hayo ya amani. Makundi hayo ni kundi la Ukombozi wa Sudan linaloongozwa na Abdelwahid al Nur na tawi la Harakati ya Ukombozi wa Sudan upande wa kaskazini (SPLM-N) inayoongozwa na Abdelaziz al Hilu.
IGAD imewapongeza wadau wote waliofanikisha kufikiwa makubaliano hayo ya amani, akiwemo Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Handook, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa nchi hiyo Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na viongozi wa makundi yote yanayobeba silaha yaliyosaini mapatano hayo.