Kundi la Haftar lakiuka makubaliano ya usitishaji vita Libya
Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya limetangaza kuwa, vikosi vya kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na Khalifa Haftar vimekiuka makubaliano ya usitishaji vita.
Jeshi la GNA limesema, vikosi vya Haftar jana Jumapili vilikiuka tena makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyofikiwa baina ya pande mbili kwa kushambulia kwa kuvilenga kwa makombora kumi vituo kadhaa vya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya, mashambulio hayo hayakusababisha maafa ya roho za watu wala hasara kwa vifaa na zana za jeshi hilo.
Tarehe 27 ya mwezi uliopita wa Agosti, vikosi vya jenerali muasi Khalifa Haftar vilikiuka kwa mara ya kwanza makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa nchini Libya kwa kushambulia kwa makombora kumi pia ngome za jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa GNA magharibi mwa mji wa Sirte.
Mnamo tarehe 21 Agosti, serikali hiyo mwafaka wa kitaifa ya Libya ilitangaza kwamba, imeanza kutekeleza usitishaji vita wa pande zote nchini humo na kwamba sharti la kudumisha usitishaji vita huo ni kutekelezwa zoezi la upokonyaji silaha katika mji huo muhimu na wa kistratejia wa Sirte.
Hata bunge la mashariki mwa Libya liliunga mkono ubunifu huo wa GNA na kusema, inapasa kuwa na mtazamo chanya kuhusiana na hatua hiyo ya kusitisha mapigano.
Hadi sasa usitishaji vita nchini Libya umesha tangazwa mara kadhaa, lakini umekiukwa na kundi la LNA linaloongozwa na Khalifa Haftar.
Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa Libya imemtuhumu Haftar mwenyewe pamoja na vikosi vyake kuwa wametenda jinai za kivita dhidi ya raia wa nchi hiyo..../