Kushadidi mgogoro wa Libya; Waziri Mkuu wa Serikali ya mashariki ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63424-kushadidi_mgogoro_wa_libya_waziri_mkuu_wa_serikali_ya_mashariki_ajiuzulu
Mgogoro wa ndani nchini Libya umeshadidi mno. Matatizo ya kiuchumi na kuvurugika maisha, kuongezeka ufisadi na kuendelea vita vya ndani kumewafanya mamia ya wananchi wa nchi hiyo katika siku za hivi karibuni kujitokeza katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kuandamana wakitaka kuhitimishwa mizozo ili kutoa fursa ya kuboreshwa hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 14, 2020 22:03 UTC
  • Kushadidi mgogoro wa Libya; Waziri Mkuu wa Serikali ya mashariki ajiuzulu

Mgogoro wa ndani nchini Libya umeshadidi mno. Matatizo ya kiuchumi na kuvurugika maisha, kuongezeka ufisadi na kuendelea vita vya ndani kumewafanya mamia ya wananchi wa nchi hiyo katika siku za hivi karibuni kujitokeza katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kuandamana wakitaka kuhitimishwa mizozo ili kutoa fursa ya kuboreshwa hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo.

Maandamano hayo ambayo yalianzia katika mji mkuu Tripoli yalisambaaa na kufika hadi mashariki mwa Libya. Kushadidi maandamano hayo kumemfanya Abdallah al-Thani, Waziri Mkuu wa serikali inayotawala mashariki mwa Libya ajiuzulu. Abdallah Bilhaq, msemaji wa Bunge la Libya la Tobruk mashariki mwa nchi ametangaza kuwa, serikali ya muda ya Abdallah al-Thani imekabidhi barua ya kujiuzulu kwa Aqila Saleh, Spika wa Bunge katika eneo hilo.

Maandamano na malalamiko katika mji mkuu Tripoli na miji ya mashariki mwa Libya ukiwemo Benghazi yameshika kasi hivi sasa. Waandamanaji wanalalamikia huduma mbovu za afya, kupungua mzunguko wa pesa taslimu sambamba na kuenea ufisadi. Kufungwa sehemu ya usafirishaji mafuta ya Libya nje ya nchi na kukaliwa kwa mabavu taasisi za mafuta na wanamgambo wenye mfungamano na jenerali muasi Khalifa Haftar ni hatua ambazo zimetoa pigo kwa vyanzo vya fedha vya serikali nchini Libya ambapo matokeo yake ni kushadidi matatizo ya kiuchumi na kukatika umeme katika akthari ya miji ya Libya.

Mapigano nchini Libya

 

Hii ni katika hali ambayo, wahandisi na maafisa wa Shirika la Umeme wametangaza kuwa, sababu ya matatizo ya umeme ni uhaba wa nishati kwa ajili ya kuendeshea vituo vya umeme na kwamba, hakuna tatizo lolote lile la kiufundi.

Katika upande mwingine, kuenea virusi vya corona nako kumekuwa na taathira hasi na mbaya kwa uchumi wa Libya. Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini Libya imekaribia 23,000 huku watu 362 wakiwa wameshaaga dunia. Katika mazingira haya, hata mashirika ya mafuta ambayo ni amilifu nchini Libya kwa sasa, katika majuma ya hivi karibuni yamesitisha shughuli zake, hatua ambayo nayo imeongeza maradufu matatizo ya nchi hiyo.

Katika majuma ya hivi karibuni kumeshuhudiwa usitishaji vita wa kiwango fulani, usitishaji vita ambao kuna uwezekanao ukakiukwa. Hili nalo ni jambo ambalo limeongeza wasiwasi wa ukosefu wa amani na usalama nchini Libya. Katika fremu hiyo, hivi karibuni kumefanyika mazungumzo yenye shabaha ya kufikia utatuzi wa kisiasa ili kuinasua nchi hiyo katika kinamasi ilichokwama ndani yake hivi sasa. Makundi mbalimbali ya Libya yalishiriki katika mazungumzo hayo huko Rabat mji mkuu wa Morocco. Pande mbili zilitangaza kuwa, zinataka kufikiwa makubaliano kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa miaka kadhaa sasa wa Libya.

Jenerali muasi Khalifa Haftar

 

Abdul-Salam al-Safrani, mjumbe wa timu ya mazungumzo ya Baraza la Uongozi la Libya linaloongozwa na Fayez al-Sarraj anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Katika mazungumzo hayo, ajenda kuu ilikuwa kuhusiana na hitilafu za kisiasa na makundi kwani ufisadi umepanuka na kushamiri mno katika nchi hiyo.

Katika wiki za hivi karibuni, waaandamamaji nchini Libya walitoa matakwa ya kisiasa pia. Wananchi hao ambao wamechoshwa na vita vya ndani baina ya makundi yanayoshikilia hatamu za uongozi nchini Libya na uingiliaji wa kigeni, wametoa wito wa kufikiwa makubaliano ili kuandaa mazingira ya kutungwa katiba, kupatikana mamlaka ya kitaifa, kuitishwa uchaguzi huru na wa wazi na kuweko vita dhidi ya ufisadi.

Baada ya mazungumzo ya Morocco, Umoja wa Mataifa unakusudia kuzialika haraka pande hasimu nchini Libya kwa ajili ya kikao maalumu cha kujadili mgogoro wa Libya huko Geneva Uswisi. Wengi wana matumaini kwamba, kikao hicho kitakuwa na matunda ya kuridhisha. Inaonekana kuwa, serikali ya mashariki mwa Libya kutokana na kupata tajiriba ya kushindwa mara kadhaa, filihali imefikia katika mkwamo ambapo viongozi wake nao sasa wanafanya juhudi ili kuhakikisha masuala yanayohusiana na nchi hiyo yanapatiwa ufumbuzi kupitia njia ya mazungumzo.

Fayez al-Sarraj, Kiongozi wa Baraza la Uongozi la Libya

 

Muhammad Khalifa Najm, mjumbewa Baraza Kuu la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa amesema: Mazungumzo yanaendelea katika mkondo chanya na mzuri na kumefikiwa maafikiano muhimu kama kuandaliwa mikakati ya kueleweka kwa ajili ya kuangamiza ufisadi na kuhitimisha migawanyiko ya asasi za serikali.

Inaonekana kuwa, kumeanza msimu mpya wa anga ya kisiasa nchini Libya. Wananchi wa Libya wamechoka na miaka mingi ya vita na uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yao ambayo yamepelekea hali ya uchumi wan chi izidi kuwa mbaya. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana wananchi wa Libya wanataka anga tulivu ya kisiasa itawale katika nchi yao, kufanyike uchaguzi na kurejeshwa amani na utulivu nchini humo. Kwa msingi huo, kujiuzulu Abdallah al-Thani, Waziri Mkuu wa Serikali ya Mashariki mwa Libya kunapaswa kutathminiwa kuwa ni hatua ya kujibu matakwa ya wananchi wenye hasira ambao hawako tayari kuvumilia hali hii inayotawala katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.