Katibu Mkuu wa UN kumteuwa mjumbe maalumu katika masuala ya Libya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limemuomba Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres kufanya uteuzi wa Mjumbe Maalumu ili kusuluhisha mzozo unaoendelea nchini Libya na kuongoza jitihada za kurejesha amani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Ghassan Salame ambaye alikuwa akiongoza ujumbe wa Umoja wa Mataifa na kusimamia jitihada za kutafuta njia za kurejesha amani huko Libya alijiuzulu mwezi Machi mwaka huu.
Miezi kadhaa iliyopita Marekani ilipendekeza kuwa, Guterres amteuwe Helle Thorning- Schmidt Waziri Mkuu wa zamani wa Denmark kuwa mjumbe wake maalumu nchini Libya. Hata hivyo wanadiplomasia walisema kuwa alijitoa mwenyewe kwenye nafasi hiyo.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa ameshtushwa na ukweli kwamba waharibifu wengi na nchi nyingi zimekuwa zikiingilia hali ya mambo huko Libya. Antonio Guterres amesema nchi ajinabi zimekuwa zikizipatia silaha pande husika katika mzozo wa Libya na kupuuza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama kuhusiana na vikwazo vya silaha na mamluki wanaopigana kwa niaba nchini humo.