Waziri Mkuu wa GNA Libya kung'atuka madarakani ifikapo mwishoni mwa Oktoba
Waziri Mkuu wa Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya GNA amesema, atajiuzulu wadhifa wake huo na kukabidhi hatamu za madaraka kwa uongozi mpya utakaochaguliwa kupitia kamati ya mazungumzo ya amani.
Fayez al Sarraj ametangaza msimamo huo katika hotuba aliyotoa kwa taifa kupitia televisheni akisisitiza kuwa mwishoni mwa mwezi ujao wa Oktoba itakuwa siku yake ya mwisho kuweko madarakani na atakabidhi madaraka kwa mamlaka mpya ya utendaji itakayochaguliwa na kamati ya mazungumzo ya amani.
Uamuzi huo wa Al Sarraj wa kukabidhi madaraka ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao unahofiwa kuwa unaweza ukaibua vita vipya vya kuwania madaraka kati ya shakhsia waandamizi ndani ya GNA na baina ya makundi ya wanamgambo wanaobeba silaha yanayounga mkono serikali hiyo.
Kiongozi huyo wa GNA, ambayo ndiyo serikali inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa amesema, mazungumzo ya usuluhishi kati ya pande hasimu za Libya ambayo yanasimamiwa na umoja huo yamefikia kwenye awamu mpya ya kuziunganisha taasisi za Libya na kufanya maandalizi kwa ajili ya chaguzi za rais na bunge.
Chini ya mashinikizo makubwa ya kimataifa, wawakilishi wa pande mbili kuu hasimu nchini Libya za Serikali ya Muafaka wa Kitaifa GNA na kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya LNA, walikutana mapema mwezi huu na kufikia makubaliano ya awali, yanayolenga kuiandaa nchi kuelekea kwenye chaguzi ndani ya kipindi cha miezi 18 ijayo na vilevile kutekeleza operesheni ya upokonyaji silaha katika mji wa Sirte.
Mji huo wa pwani ambao unadhibitiwa na kundi la LNA linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar ndio njia kuu ya kuvifikia visima vikubwa vya mafuta vya Libya na vituo vikuu vya kusafirishia bidhaa hiyo nje ya nchi.
Tangu mwezi Januari, kundi hilo la Jeshi la Taifa la Libya limezuia usafirishaji wa nishati hiyo nje ya nchi na hivyo kuifungia na kuikosesha Libya chanzo chake kikuu cha mapato. Hatua hiyo ya LNA imesababisha hali ya maisha ya raia kuwa mbaya zaidi na kuchochea maandamano ya malalamiko na upinzani katika miji inayodhibitiwa na pande zote hizo mbili hasimu katika mgogoro wa Libya.../