Libya na Uturuki zasisitiza kuhusu uhusiano wa karibu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63835-libya_na_uturuki_zasisitiza_kuhusu_uhusiano_wa_karibu
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekutana na Waziri Mkuu wa Libya anayeondoka Fayez al-Sarraj, ambaye anaongoza Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA), inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 05, 2020 09:37 UTC
  • Libya na Uturuki zasisitiza kuhusu uhusiano wa karibu

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekutana na Waziri Mkuu wa Libya anayeondoka Fayez al-Sarraj, ambaye anaongoza Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA), inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Viongozi hao wawili wakiwa wameandamana na maafisa wa ngazi za juu kutoka pande mbili, wakiwemo mawaziri wa ulinzi, mambo ya nje , mambo ya ndani na fedha pamoja na washauri waandamizi, walifanya mazungumzo katika mji wa Istanbul nchini Uturuki siku ya Jumapili.

Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu mkutano huo isipokuwa taarifa iliyosema kuwa pande mbili zina mpango wa kuimarisha zaidi uhusiano.

Mwezi Septemba  mjini Istanbul kulifanyika mkutano mwingine baina ya Erdogan na Sarraj ambaye anapanga kuachia ngazi mwezi huu.

Uturuki na Libya zimewahi kutia saini mapatano ya kijeshi na ushirikiano katika masuala ya Bahari ya Mediterranea.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao makuu yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar ambaye ni kinara wa wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya, na nyingine ya Mwafaka wa Kitaifa, yenye makao yake Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Mwaka jana, al Sarraj alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki mjini Ankara na baada ya hapo Uturuki ilituma wanajeshi wake nchini Libya kuisaidia Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.

Kwa upande wake, wanamgambo wa "Jeshi la Taifa la Libya" wanaungwa mkono na mahasimu wakubwa wa Uturuki yaani Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi.