Umoja wa Afrika wapongeza makubaliano ya kusitisha vita nchini Libya
-
Moussa Faki
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amepongeza makubaliano ya kukomesha vita na mapigano nchini Libya akiyataja kuwa ni hatua muhimu katika njia ya kurejesha amani katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Taarifa iliyotolewa na Moussa Faki Mahamat imesema kuwa, utatuzi wa kisiasa unaopatikana kwa njia ya mazungumzo na mapatano ya kitaifa ndivyo vinavyoweza kutatua matatizo ya wananchi wa Libya.
Umoja wa Afrika pia umezitaka pande zote za mgogoro wa Libya kujiunga na makubaliano ya amani ya Geneva na kuheshimu mapatano hayo.
Hatimaye baada ya mazungumzo marefu na tata, pande hasimu nchini Libya Ijumaa iliyopita zilitiliana saini makubaliano ya usitishaji vita chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.
Makubaliano hayo yanawataka wanajeshi na wapignaji wote wa nchi ajinabi kuondoka katika ardhi ya Libya katika kipindi cha miezi mitatu.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Libya, Stephanie Williams pia ameeleza matarajio kwamba makubaliano hayo yanaweza kuhitimisha matatizo ya muda mrefu ya wananchi wa Libya.
Libya ilitumbukia katika lindi la vita na mapigano ya ndani mwaka 2011 baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.