Wafanyakazi wa Sudan nchini UAE wanahadaiwa kuingia vitani Libya
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limefichua kuwa mamia ya raia wa Sudan wanaofanya kazi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wamehadaiwa kuingia vitani Libya na kujiunga na wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar.
Taarifa hiyo imesema shirika la huduma za usalama la Black Shield Security Services limewaajiri Wasudani 390 ambao walihadaiwa kuwa wanaenda kufanya kazi kama walinzi nchini UAE lakini sasa wamejipata vitani Libya.
Baada ya Wasudan hao kuwasili katika uwanja wa ndege wa Abu Dhabi hupelekwa katika kituo cha kijeshi baada ya kupokonywa pasipoti zao. Msudani mmoja aliyehojiwa na ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema badala ya kufanya kazi kama walinzi wa kawaida katika maduka au idara nchini UAE walipata mafunzo ya kijeshi na kisha wakapalekwa katika mji wa Ras Lanuf nchini Libya kujiunga na wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye anataka kuiangusha serikali halali ya Libya yenye makao yake Tripoli.
Umoja wa Falme za Kiarabu hukiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa vya silaha dhiri ya Libya ambavyo vilianza kutekelezwa mwaka 2011. UAE imekuwa ikimpa silaha Haftar na kumsaidia katika oparesheni zake dhidi ya serikali ya Libya.
Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.