Nov 29, 2020 07:49 UTC
  • Kwa akali wakulima 43 wauawa na Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria

Maafisa wa serikali ya Nigeria wametangaza kuwa, kwa akali watu 43 wameuawa kikatili kufuatia mashambulio yaliyofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Taarifa ya maafisa wa serikali ya Nigeria imeeleza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram jana walifanya mashambulio makubwa kwenye kijiji cha Kashobe katika jimbo la Borno na kuwauawa kwa akali wakulima 43.

Hadi sasa jeshi au polisi ya Nigeria haijatoa radiamali yoyote kuhusiana na mauaji hayo ya jana ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

mauaji hayo yanatokeo siku chache tu baada ya jeshi la Nigeria kutangaza habari ya kuuawa makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Katika majuma ya hivi karibuni kundi  la Boko Haram limezidisha mashambulio yake katika maeneo mbalimbali ya umma hususan kaskazini mashariki mwa Nigeria na kusababisha hasara kubwa za mali na roho za watu.

Wanachama wa Boko Haram

 

Kundi hilo lilianzisha harakati zake za kigaidi mwaka 2009 huko kaskazini mwa Nigeria na hadi sasa limepanua hujuma na mashambulizi hayo katika nchi kama Cameroon, Chad na Niger.

Maelfu ya watu wameuawa katika mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi katika nchi hizo.

Serikali ya Nigeria inalaumiwa kwa kuzembea kuliangamiza kundi hilo la kigaidi licha ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo kuahidi kwamba, moja ya majukumu muhimu ya utawala wake ni kulisambaratisha kikamilifu kundi hilo. 

Tags