Walioaga dunia kwenye mkasa wa kuporomoka jengo Nairobi, Kenya wafikia 49
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6676-walioaga_dunia_kwenye_mkasa_wa_kuporomoka_jengo_nairobi_kenya_wafikia_49
Habari kutoka Nairobi, mji mkuu wa Kenya zinasema idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye mkasa wa kuporomoka jengo mtaani Huruma jijini hapo imefikia watu 49, huku familia 191 zilizoathirika zikipewa hifadhi na shirika la Msalaba Mwekundu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2016 10:38 UTC
  • Walioaga dunia kwenye mkasa wa kuporomoka jengo Nairobi, Kenya wafikia 49

Habari kutoka Nairobi, mji mkuu wa Kenya zinasema idadi ya watu waliopoteza maisha kwenye mkasa wa kuporomoka jengo mtaani Huruma jijini hapo imefikia watu 49, huku familia 191 zilizoathirika zikipewa hifadhi na shirika la Msalaba Mwekundu.

Japheth Koome, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi jijini humo amesema miili 7 imeondolewa kwenye vifusi vya jengo hilo na hivyo kupelekea idadi ya walioaga dunia katika tukio hadi sasa kufikia watu 49.

Huku hayo yakijiri, Gavana wa kaunti ya Nairobi Dakta Evans Kidero ametoa agizo la kusimamishwa shughuli ya kubomoa majengo hafifu katika mtaa wa Huruma kwa muda wa siku saba ili kutoa nafasi kwa wapangaji kutafuta makaazi mbadala.

Nyumba kadhaa zilibomolewa kati ya Ijumaa na jana Jumamosi katika mtaa huo na kusababisha mamia ya familia kulala nje kwenye baridi kali wasijue pa kwenda. Habari zinasema kuwa, familia 191 zilizoathirika na mkasa huo kwa sasa zinapewa hifadhi kwenye kambi ya muda na shirika la Msalaba Mwekundu jijini Nairobi.

Makumi ya watu hawajulikani waliko baada ya jengo hilo ambalo limejengwa karibu na mto kuporomoka usiku wa Aprili 29.

Waokoaji wakiwemo maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu, wanajeshi na vijana wa shirika la NYS wangali wanaendelea kupekua vifusi wakitafuta walionusurika au miili iliyo katika eneo hilo.