Apr 13, 2021 06:51 UTC
  • Rais Ramaphosa ataka Afrika ianze kujizalishia chanjo ya Covid-19

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema bara la Afrika linahitaji ujuzi na uwezo wa kujitengenezea chanjo za kupambana na ugonjwa wa Covid-19, wakati huu ambapo bara hilo linakumbwa na uhaba mkubwa wa chanjo hizo.

Rais Ramaphosa alisema hayo jana Jumatatu katika kongamano la Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Umoja wa Afrika (Afrika-CDC) lililojadili suala la uzalishaji wa chanjo za kukabiliana na virusi vya Corona; ambapo alieleza kuwa, "Bara Afrika linahitaji kukumbatia uwezo wake, na litambue fursa za ushirikiano miongoni mwa nchi za bara hilo."

Rais wa Afrika Kusini amebainisha kuwa, baadhi ya nchi kama Brazil na India zinaweza kulipa bara Afrika ujuzi na uzoefu wa kuboresha sekta ya madawa ya bara hilo.

Kauli ya Ramaphosa imepigwa jeki na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye pia ameliambia kongamano hilo kuwa, usawa katika ugavi wa chanjo za Corona hauwezi kudhaminiwa na irada njema tu, lakini bara Afrika linahitaji uwezo wa kujitengenezea chanjo na madawa yake.

Chanjo ya Corona

Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Umoja wa Mataifa (UN) kwa mara kadhaa zimekosoa ugawaji usio wa kiadilifu wa chanjo za Corona duniani.

WHO na UN zinasisitiza kuwa, mgogoro unaoikabili dunia hivi sasa unahitajia jibu la kimataifa, na kwamba ufumbuzi wa suala la ugavi wa chanjo unahitaji umoja na ushirikiano kwa nchi mbalimbali duniani. 

 

Tags