Askari usalama Nigeria wawakamata wanachama 40 wa genge lenye silaha
(last modified Tue, 27 Apr 2021 07:16:39 GMT )
Apr 27, 2021 07:16 UTC
  • Askari usalama Nigeria wawakamata wanachama 40 wa genge lenye silaha

Kikosi cha usalama nchini Nigeria ckimewatia nguvuni wanachama 40 wa genge la watu waliokuwa na silaha wakati wa operesheni iliyofanyika katika jimbo la kusini la Edo.

Taarifa iliyotolewa na George Edem, kamanda wa Kikosi cha Usalama na Ulinzi wa Wananchi huko Edo, amesema idadi kubwa ya risasi za genge hilo pia zilikamatwa katika operesheni iliyofanyika katika mji wa Benin ambao ni makao makuu ya jimbo la Edo.

Mgogoro ulioanza mnamo 2008 kati ya wafugaji wa ng'ombe na wakulima umegeuka kuwa operesheni za utekaji nyara na ujambazi katika maeneo hayo ya Nigeria.
Mwaka jana, zaidi ya watu 3,000 walipoteza maisha nchini humo kwa sababu ya mapigano ya silaha kati ya magenge tofauti.

Jumanne iliyopita pia watu waliokuwa na silaha waliteka nyara idadi isiyojulikana ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Greenfield na kumuua kwa risasi mwalimu mmoja wa chuo hicho. 

Magenge yenye silaha yanateka nyara raia Nigeria

Hadi leo hii idadi hasa ya watu waliotekwa nyara katika chuo kikuu hicho haijajulikana. Hilo ndilo tukio la karibuni zaidi la utekaji nyara katika nchi hiyo ambayo imeshamiri vitendo hivyo viovu.

Magenge ya watu wenye silaha yaliyopachikwa jina la majambazi yamekuwa yakiteka nyara wanafunzi mara kwa mara na kudai vikomboleo nchini Nigeria. Tangu mwezi Disemba 2020, mamia ya wanafunzi wametekwa nyara nchini humo kutokana na udhaifu mkubwa wa taasisi za kulinda usalama wa raia.