May 06, 2021 12:42 UTC
  • ICC yamhukumu Ongwen kifungo cha miaka 25 jela

Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wamemhukumu kifungo cha miaka 25 jela Dominic Ongwen, mwanajeshi mtoto wa zamani wa Uganda ambaye alikuwa kamanda wa kundi la waasi wa Lords Resistance Army (LRA), baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu nchini Uganda.

Wahanga wa jinai za Ongwen walikuwa wameiomba mahakama hiyo ya mjini Hague nchini Uholanzi imhukumu kifungo cha maisha jela mbabe huyo wa kivita, huku timu ya mawakili wa kiongozi huyo wa zamani wa waasi ikitaka mteja wao afungwe miaka 10 jela, ikisisitiza kuwa, alilazimishwa kuingia jeshini akiwa mtoto mdogo.

Ongwen aliyekamatwa mwaka 2015 alieleza jinsi alivyotekwa nyara na wapiganaji wa Joseph Kony mnamo mwaka 1987 alipokuwa akienda shule. Februari mwaka huu, kiongozi huyo wa waasi alipatikana pia na hatia ya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono na kuwasajili kwa nguvu watoto kujiunga na kundi hilo la waasi.

Kwa mujibu wa Waendesha Mashitaka wa ICC, Ongwen mwenye umri wa miaka 45 aliamuru kushambuliwa kambi za wakimbizi mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati alipokuwa mmoja wa makamanda wa kundi la waasi wa LRA, linaloongozwa na mbabe wa kivita Joseph Kony, ambaye aliongoza vita vya kinyama nchini Uganda na katika nchi tatu jirani ili kuunda taifa litakalofuata misingi na amri kumi za Biblia.

Ongwen alipokuwa mwanajeshe mtoto (kulia) na hivi sasa kizimbani ICC

Kundi la waasi wa Kikristo wa LRA  wa nchini Uganda wanaoongozwa Joseph Kony limekuwa likitekeleza jinai kaskazini mwa Uganda kwa zaidi ya miaka 20 kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Rais Yoweri Museveni.

Waasi hao ambao wamepanua wigo wao hadi katika nchi jirani sasa wamedhoofika na wanakaribia kuangamizwa kikamilifu.

Tags