Hollande: Askari wa Ufaransa tayari wamemaliza kipindi cha kuhudumu nchini CAR
Rais François Hollande wa Ufaransa amesema kuwa, askari wa nchi yake wamemaliza kipindi cha kuhudumu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na wataanza kuondoka mwishoni mwa mwaka huu.
Rais Hollande ameyasema hayo katika safari yake ya masaa machache nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo aliongeza kuwa, askari wa Ufaransa wataanza kuondoka nchini humo mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu. Katika safari hiyo rais huyo wa Ufaransa amedai kuwa, operesheni za Sangaris zinazotekelezwa na askari wa nchi yake kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa zimekuwa na mafanikio makubwa. Aidha ameongeza kuwa, Paris iliamua kuchukua uamzi wa kutuma askari hao nchini humo mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka 2013, kufuatia kuibuka machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hii ni katika hali ambayo gazeti la Kifaransa la Le Figaro limeandika kuwa, ni mara kadhaa sasa askari wa Ufaransa wamekuwa wakituhumiwa kufanya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo na wanawake nchini CAR na kwamba hadi sasa faili za tuhuma zao bado liko wazi katika vyombo vya mahakama vya Ufaransa. Wakati huo huo serikali ya Paris imekusudia kuongeza idadi ya askari wake nchini Kodivaa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, askari wa Ufaransa watatumwa nchini Ivory coast kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuimarisha ulinzi wa eneo la Sahel na kuzisaidia operesheni za kupambana na ugaidi maarufu kwa jina la opereseheni za Barkhan. Operesheni hizo zitaandaa mazingira ya kutumwa askari 3500 wa Ufaransa katika nchi za Mali, Mauritania, Niger, Chad na Burkina Faso.