Jeshi la Msumbiji latuhumiwa kujihusha na vitendo vya mauaji na ubakaji
Jeshi la Msumbiji linatuhumiwa kuhusika na vitendo vya mauaji na ubakaji dhidi ya raia.
Mtandao wa Habari wa al-Yaum Sab'i umelinukuu gazeti moja la Msumbiji na kuandika kuwa, maelfu ya raia wa nchi hiyo waliokimbilia Malawi kuepuka machafuko ya nchi yao wanasema kuwa, wanajeshi wa Msumbiji wanaua raia na kuwabaka. Gazeti hilo la Malacha linaripoti kwamba, jeshi la Msumbiji limekuwa likiviteketeza kwa moto vijiji vya nchi hiyo ambavyo wanadhani vina wapinzani wanaobeba silaha.
Mashuhuda wanasema kwamba, jeshi la Msumbiji limekuwa likivamia hata maeneo ya kuhifadhi chakula na mazao na kuyachoma moto. Hata hivyo, serikali ya Maputo imeripotiwa ikikanusha vikali madai hayo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) limearifu kuwa, mapigano ya wiki za hivi karibuni baina ya askari wa chama tawala Frelimo na wale wa chama kikuu cha upinzani Renamo, yamewalazimisha maelfu ya raia kuyahama makazi yao na kukimbilia katika nchi jirani ya Malawi.
Msumbiji imekuwa ikitawaliwa na chama cha Frelimo tangu ilipopata uhuru na kiongozi wa waasi wa zamani wa Renamo Afonso Dhlakama amekuwa akishindwa katika uchaguzi wa rais tangu mwaka 1994 na chama hicho kubakia kuwa harakati kuu ya upinzani.