Aug 13, 2021 23:59 UTC
  • Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kufungua ofisi Sudan

Sudan na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake huko Hague, Uholanzi zimesaini makubaliano ya ushirikiano kama hatua moja mbele katika jitihada za kushughulikia kesi ya dikteta wa zamani wa Sudan, Omar Hassan al Bashir ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika jimbo la Darfur, magharibi mwa Sudan.

Karim Khan Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo, ambaye amevitaja vita vya ndani katika jimbo la Darfur kuwa ni "ukurasa mweusi" katika historia ya Sudan ameeleza kuwa, mipango inafanyika ili mahakama ya ICC ifungue ofisi yake huko Sudan kwa ajili ya kukusanya ushahidi zaidi na hivyo kuwa na hoja zenye mashiko katika kesi ya al Bashir. 

Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC 

Al Bashir mwenye umri wa miaka 77 anasakwa na mahakama ya ICC kwa zaidi ya muongo mmoja sasa kwa tuhuma za mauaji ya kimbari, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Darfur. Wasaidizi wawili wa kiongozi huyo wa zamani wa Sudan pia wanasakwa kwa kutenda jinai za kivita katika jimbo hilo. 

Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa, watu laki tatu waliuliwa na wengine milioni mbili na laki tano kulazimika kuyahama makazi yao katika machafuko na vita vilivyolikumba jimbo la Darfur mwaka 2003.

Sudan imekuwa ikiongozwa na serikali ya mpito ya kijeshi tangu Agosti mwaka 2019. Serikali hiyo imeahidi kuwatendea haki wahanga wa jinai zilizojiri wakati wa utawala wa al Bashir. Juzi Alhamisi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC aliwaambia waandishi wa habari huko Khartoum kwamba, ameridhishwa na ripoti kuwa serikali ya mpito ya Sudan imesaini makubaliano mapya ya ushirikiano na ofisi yake.

Rais wa zamani wa Sudan, Omar Hassan al Bashir ambaye alitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu kabla ya kuenguliwa madarakani kufuatia maandamano ya wananchi mwaka 2019, sasa yuko gerezani katika jela yenye ulinzi mkali ya Kober huko Khartoum. 

Tags