Harakati ya Ennahda Tunisia yapinga maamuzi ya Rais Kais Saied
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75234-harakati_ya_ennahda_tunisia_yapinga_maamuzi_ya_rais_kais_saied
Harakati ya Ennahda nchini Tunisia imepinga hatua ya rais wa nchi hiyo ya kumteua waziri mkuu mpya ikisema kuwa ni sawa na kukanyaga katiba ya nchi na kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa sheria na demokrasia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2021 07:59 UTC
  • Harakati ya Ennahda Tunisia yapinga maamuzi ya Rais Kais Saied

Harakati ya Ennahda nchini Tunisia imepinga hatua ya rais wa nchi hiyo ya kumteua waziri mkuu mpya ikisema kuwa ni sawa na kukanyaga katiba ya nchi na kufanya mapinduzi dhidi ya utawala wa sheria na demokrasia.

Taarifa ya chama hicho kikubwa zaidi cha saisa nchini Tunisia imetolewa baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kumteua Najla Bouden Romdhane, kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi hiyo, karibu miezi miwili tangu alipohodhi madaraka yote ya nchi hiyo. 

Taarifa ya chama hicho imepinga vikali hatua ya mtu mmoja kujipa mamlaka ya kusitisha shughuli za Serikali, Bunge la Mahakama na kutaka kulazimisha maoni na matakwa yake.

Taarifa ya Harakati ya Ennahda imeyataka makundi yote bungeni, wanasiasa huru na makundi ya kitaifa kushikamana na kulinda demokrasia ya Tunisia.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tunisia mwanamke kuteuliwa kuwa waziri mkuu. 

Bouden, (63) anakuwa waziri mkuu wa 11 wa Tunisia tangu mapinduzi ya mwaka 2011 

Bi Bouden, ambaye ni mhandisi wa chuo kikuu asiye na umaarufu, anashika wadhifa huo mpya wa uwaziri mkuu wakati Tunisia imegubikwa na wingu zito la mgogoro wa kitaifa, ambao umeyatia mashakani mafanikio ya kidemokrasia yaliyopatikana kupitia mapinduzi ya umma ya mwaka 2011.

Mwezi Julai mwaka huu Rais Kais Saied alimuuzulu waziri mkuu, akalisimamisha Bunge na kuhodhi madaraka yote ya utendaji. Tangu wakati huo amekuwa akishinikizwa ndani ya nchi na kimataifa aunde serikali mpya.

Wanasiasa nchini Tunisia wamezitaja hatua za karibuni za Rais Kais Saied kuwa ni kuhodhi madaraka ya nchi na wakati huo huo wametahadharisha juu ya uwezekano wa Tunisia kurejea katika zama za udikteta.