Rais wa zamani ataka maandamano makubwa dhidi ya Rais wa sasa Tunisia
Aliyekuwa rais wa Tunisia amewataka wananchi wa hiyo ya Kiarabu kushiriki kwa wingi katika maandamano yanayotazamiwa kufanyika leo Jumapili, dhidi ya rais wa sasa wa hiyo, Kais Saied, anayemtuhumu kuwa amehodhi madaraka na mamlaka yote ya nchi.
Moncef Marzouki ametoa mwito huo katika kanda fupi ya video iliyotumwa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook, ambapo amesema: Nawaasa Watunisia wote kuandamana Jumapili kwa ajili ya kulinda katiba, demokrasia, uhuru, na mamlaka ya kitaifa ya kujitawala.
Marzouki amewataka wananchi wa Tunisia washiriki kwa wingi kwenye maandamano ya leo pasi na kujali mirengo yao ya kisiasa, akisisitiza kuwa hawajahi kuiona Tunisia maishani mwake kama ilivyo hivi sasa, na kwamba umewadia wakati wa kuchukua hatua.
Haya yanajiri wiki moja baada ya zaidi ya watu elfu tano kushiriki maandamano ya kumuunga mkono Rais Kais Saied anayetuhumiwa na upinzani kuhodhi madaraka yote ya utendaji ya nchi hiyo.
Tarehe 26 Julai, Rais Kais Saied alimuuzulu Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kulisimamisha pia bunge la nchi hiyo. Sambamba na hatua hiyo, aliwaondolea wabunge kinga ya kisheria.
Wanasiasa nchini Tunisia wamezitaja hatua za karibuni za Rais Kais Saied kuwa ni kuhodhi madaraka ya nchi na wakati huohuo wametahadharisha juu ya uwezekano wa Tunisia kurejea katika zama za udikteta.