Maelfu ya watu waandamana nchini Tunisia kutaka Rais Kais Saied ajiuzulu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i75618-maelfu_ya_watu_waandamana_nchini_tunisia_kutaka_rais_kais_saied_ajiuzulu
Maelfu ya watu wamemiminika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Tunisia, Tunis katika maandamano mapya ya kumtaka rais wa nchi hiyo Kais Saied ajiuzulu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 10, 2021 23:01 UTC
  • Maelfu ya watu waandamana nchini Tunisia kutaka Rais Kais Saied ajiuzulu

Maelfu ya watu wamemiminika kwenye mitaa ya mji mkuu wa Tunisia, Tunis katika maandamano mapya ya kumtaka rais wa nchi hiyo Kais Saied ajiuzulu.

Maandamano hayo ya maelfu ya Watunisia yamefanyika siku ya Jumapili katika mitaa mbalimbali chini ya ulinzi mkali wa askari wa vikosi vya usalama.

Hata kabla ya kuwasili kwenye mtaa wa Bourguiba, ambalo ndilo eneo kuu la maandamano hayo dhidi ya Rais Saied, maelfu ya maafisa wa polisi walikuwa tayari wamezingira eneo hilo. 

Mamlaka za serikali zilikuwa zimepiga marufuku maandamano hayo kufanyika katika baadhi ya mitaa, na vilevile marufuku kwa waandishi wa habari kukaribia maandamano hayo. Maafisa wa polisi waliokuwa wamepiga kambi karibu na eneo la maandamano waliwataka waandamanaji warudi nyuma.

Maandamano ya jana yamefanyika huku aliyekuwa rais wa Tunisia Moncef Marzouki akiwa amewataka wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu kushiriki kwa wingi katika maandamano hayo.

Rais Kais Saied

Maandamano hayo yamefanyika wiki moja baada ya zaidi ya watu elfu tano kushiriki maandamano ya kumuunga mkono Rais Kais Saied anayetuhumiwa na upinzani kuhodhi madaraka yote ya utendaji ya nchi hiyo.

Tarehe 26 Julai, Rais Kais Saied alimuuzulu Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kulisimamisha pia bunge la nchi hiyo. Sambamba na hatua hiyo, aliwaondolea wabunge kinga ya kisheria.

Hatimaye tarehe 29 ya mwezi uliopita wa Septemba rais huyo wa Tunisia alimteua Najla Bouden Romdhane kuwa waziri mkuu na kumpa jukumu la kuunda serikali.

Saied alitangaza pia kwamba, waziri mkuu huyo mpya wa kwanza mwanamke ataongoza serikali hadi mwishoni mwa kipindi cha sheria ya hali ya hatari aliyoweka nchini humo.../