Rais wa Tunisia aahidi kuanzisha mazungumzo ya kitaifa nchini
Rais Kais Saied wa Tunisia amesema kuwa karibuni ataanzisha mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho katiba na mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Rais Saied amesema kupitia ukurasa wake wa mtandao kijamii wa Facebook kuwa vijana wa nchi hiyo pia watashirikishwa kwenye mazungumzo hayo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Kais Saied amezitahadharisha nchi za kigeni kutoingilia mambo ya ndani ya Tunisia na kuyataka madola makubwa ambayo yamezuia fedha za nchi hiyo katika benki zao, fedha ambazo ziliwekwa kwenye benki hizo kwa njia zisizo za kisheria, kuwarejeshea Watunisia fedha hizo mara moja.
Kwa sasa Tunisia inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa na kiuchumi kufuatia uamuzi usio wa kawaida uliochukuliwa na Rais Kais Saied tarehe 25 Julai na Septemba 22 mwaka huu wa kusimamisha kwa muda shughuli za bunge, kufutilia mbali kinga ya wabunge, kusimamisha shughuli za tume inayosimamia katiba, kumfuta kazi Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kusimamia mwenyewe shughuli ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali ya Tunisia.