Moncef Marzouki: Saeid auzuliwe na kushtakiwa kwa kuangamiza utawala wa Sheria Tunisia
-
Moncef Marzouki
Rais wa zamani wa Tunisia amewataka wananchi wa nchi hiyo wafanye maandamano ya kupinga maamuzi ya rais wa sasa wa nchi hiyo, Kais Saied, kumuondoa madarakani na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kuangamiza serikali, mapinduzi ya wananchi na utawala wa sheria.
Moncef Marzouki amesema kuwa, Kais Saied ameangamiza serikali na utawala wa sheria kupitia maamuzi yake na sasa anafanya mikakati ya kuiangamiza Tunisia kwa kutunga sheria mpya ya uchaguzi ambayo amesema tajiriba imethibitisha kuwa itashindwa.
Marzouki pia amewataka Watunisia kufanya mapambano ya amani dhidi ya mipango na maamuzi ya rais wa sasa wa nchi hiyo na kumfikisha mahakamani yeye na wasaidizi wake. Amesisitiza kuwa, kura ya maoni iliyopangwa kuitishwa na kiongozi huyo inakusudia kupasisha “kibali cha kifo cha utawala wa sheria” nchini Tunisia.
Rais wa zamani wa Tunisia ameyataka makundi na vyama mbalimbali vya nchi hiyo kutupilia mbali hitilafu zao za kisiasa na kushirikiana kwa ajili ya lengo moja la kuikoa nchi, utawala wa sheria na Katiba.
Tunisia ilitumbukia katika mivutano na mgogoro mkubwa wa kisiasa tangu tarehe 25 Julai wakati Rais wa nchi hiyo, Kais Saied alipoanza kuchukua maamuzi yanayotajwa kuwa yanapingana na Katiba ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za Bunge, kuwaondolea wabunge kinga ya kisheria, kumuuzulu waziri mkuu wa nchi hiyo na kuhodhi madaraka yote ya nchi.
Makundi na vyama vya siasa nchini Tunisia vinapinga maamuzi hayo na vinayataja kuwa ni mapinduzi dhidi ya Katiba.