Financial Times: Fungate ya Rais Kais Saied wa Tunisia inaelekea ukingoni
-
Rais Kais Saied wa Tunisia
Gazeti la Financial Time la Uingereza limeripoti kuwa wataalamu wanasema fungate ya Rais wa Tunisia itamalizika hivi karibuni kutokana na mashaka ya kushindwa kwake kupata suluhisho la haraka la mgogoro wa kiuchumi unaoisumbua nchi hiyo licha ya kuwa na uungaji mkono wa kiasi fulani kwa sasa.
Ripoti ya gazeti hilo la Uingereza imesema kuwa Rais Kais Saied wa Tunisia atalazimika kulegeza kamba na kuwakumbatia wanasiasa mashuhuri na Jumuiya ya Wafanyakazi kutokana na mashinikizo makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kuhofia machafuko makubwa zaidi na malalamiko ya wananchi wanaosumbuliwa na hali ngumu ya maisha.
Gazeti hilo limewanukuu wachambuzi wa masuala ya ndani wa Tunisia wakisisitiza kuwa Kais Saied yumkini akakabiliwa na wimbi kubwa la mapinduzi ya wananchi litakalosomba kila kitu kutokana na hali mbaya ya kiuchumi na kwamba kiongozi huyo atajikuta mbele ya machaguo mawili ambayo ni ama kufanya mazungumzo na makundi mengine ya kisiasa au kutumia mkono wa chuma kwa ajili ya kukandamiza harakati ya wananchi.
Ripoti hiyo imeashiria kwamba wabunge na wanasiasa wengi wa Tunisia walijikuta katika kifungo cha nyumbani na kuzuiwa kufanya safari nje ya nchi baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Rais Kais Saied wa Tunisia. Vilevile imeashiria ukandamizaji wa uhuru wa kiraia na kubinywa vyombo vya habari na kusema serikali ya sasa ya Tunisia imefunga vituo viwili vya runinga vinavyomilikiwa na vyama viwili vikubwa vya siasa kwa kisingizio cha kutokuwa na vibalii.
Vilevile inaendelea kuwaandama wanasiasa mashuhuri na hjivi karibuni ilitoa kibali cha kimataifa cha kutiwa nguvuni rais wa zamani wa nchi hiyo, Moncef Marzouki aliyekosoa udikteta wa Rais Kais Saied na kutoa wito wa kumuondoa madarakani na kumfikisha mahakamani kwa tuhuma za kuangamiza serikali, mapinduzi ya wananchi na utawala wa sheria.