Mabrouk: Tunisia sasa iko nje ya klabu ya mataifa ya kidemokrasia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i77892-mabrouk_tunisia_sasa_iko_nje_ya_klabu_ya_mataifa_ya_kidemokrasia
Waziri wa zamani wa Tunisia ameseaa kuwa nchi hiyo imeachana na klabu ya nchi za kidemokrasia baada ya rais wa nchi hiyo kutwaa mamlaka yote ya utendaji mapema mwaka huu, na kusababisha mzozo mkubwa wa kisiasa nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 11, 2021 08:09 UTC
  • Mabrouk: Tunisia sasa iko nje ya klabu ya mataifa ya kidemokrasia

Waziri wa zamani wa Tunisia ameseaa kuwa nchi hiyo imeachana na klabu ya nchi za kidemokrasia baada ya rais wa nchi hiyo kutwaa mamlaka yote ya utendaji mapema mwaka huu, na kusababisha mzozo mkubwa wa kisiasa nchini humo.

Akizunguzma katika mahojiano na shirika la habari la Anadolu, waziri wa zamani wa utamaduni wa Tunisia, Mehdi Mabrouk amesema kuwa mgogoro wa kisiasa umeongezeka nchini Tunisia na kudhoofisha tajiriba ya mpito ya kidemokrasia katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika inayotajwa kuwa taifa pekee lililofanikiwa kufanya hivyo baada ya vuguvugu la Msimu wa Machipuo wa Kiarabu hapo mwaka 2011.

Mabrouk, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kiarabu cha Utafiti na Mafunzo ya Sera nchini Tunisia amesema: "Tangu Rais Kais Saied alipolitimua baraza la mawaziri, kusimamisha Bunge, na kutwaa mamlaka yote ya utendaji Julai 25, nchi imekuwa katika mpasuko wa kijamii. 

Amesema kiwango cha uhuru nchini Tunisia kimeshuka chini akitaja "ongezeko la idadi ya watu waliokamatwa, kesi za raia katika mahakama za kijeshi, kusimamishwa kwa Katiba, kubinywa kwa Baraza Kuu la Mahakama, kufungwa idadi ya mashirika ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Kupambana na Rushwa, na zuio la maandamano" kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya kupungua uhuru wa kijamii nchini Tunisia.

Waziri wa zamani wa utamaduni wa Tunisia pia amegusia suala la ushiriki wa majeshi ya nchi hiyo katika siasa na kusema: "Labda tutahitaji miaka mingi kugundua ukweli wa jambo hilo, lakini dalili zote zinaonyesha kuwa jeshi limesukumwa na kulazimishwa kuingilia moja kwa moja masuala ya siasa, na mapinduzi ya sasa yasingefanyika bila idhini ya jeshi."

Tarehe 26 Julai, Rais Kais Saied alimuuzulu Waziri Mkuu Hichem Mechichi na kulisimamisha pia bunge la nchi hiyo. Sambamba na hatua hiyo, aliwaondolea wabunge kinga ya kisheria.