Rais wa Tunisia: Bunge linaendelea kusitishwa hadi uchaguzi mpya utakapoandaliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78010-rais_wa_tunisia_bunge_linaendelea_kusitishwa_hadi_uchaguzi_mpya_utakapoandaliwa
Rais wa Tunisia Kais Saied alitangaza jioni ya Jumatatu jana kwamba Bunge la nchi hiyo litaendelea kusitishwa hadi uchaguzi mpya utakapoandaliwa, akiyashutumu makundi ya kisiasa kuwa yamesaliti nchi na kupora fedha za umma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 13, 2021 23:53 UTC
  • Kais Saied
    Kais Saied

Rais wa Tunisia Kais Saied alitangaza jioni ya Jumatatu jana kwamba Bunge la nchi hiyo litaendelea kusitishwa hadi uchaguzi mpya utakapoandaliwa, akiyashutumu makundi ya kisiasa kuwa yamesaliti nchi na kupora fedha za umma.

Saied alitangaza - katika hotuba ya televisheni kutoka Ikulu ya Carthage - kwamba ataandaa mashauriano ya umma kupitia majukwaa ya kijamii kuanzia Januari hadi Machi 20 mwaka ujao na kwamba ataunda kamati ambayo itakusanya na kuratibu mapendekezo ya wananchi na itakamilisha kazi yake mwisho mwa mwezi Juni mwakani.

Rais wa Tunisia ameongeza kuwa rasimu ya mageuzi ya Katiba na Sheria ya Uchaguzi, miongoni mwa mambo mengine, itawasilishwa kwenye kura ya maoni tarehe 25 Julai.

Saied amesisitiza kuwa, wale wote waliofanya jinai dhidi ya nchi na watu wa Tunisia tangu wakati wa mapinduzi nchini humo watahukumiwa, akitoa wito kwa mahakama kutekeleza majukumu yake ndani ya fremu ya kutoegemea upande wowote.

Inafaa kukumbusha kuwa, tangu Julai 25 mwaka huu, Tunisia imekuwa ikishuhudia mzozo wa kisiasa baada ya Rais Kais Saied wa nchi hiyo kuchukua hatua za kipekee, ikiwa ni pamoja na kulivunja Bunge, kuondoa kinga ya wabunge, kufuta chombo cha ufuatiliaji wa Katiba, kumfukuza Waziri Mkuu na kutwaa madaraka yote ya nchi.

Vyama vingi vya siasa nchini Tunisia vimepinga maamuzi ya kipekee ya Kais Saied na vinayataja kuwa ni "mapinduzi dhidi ya Katiba."