Waziri Mkuu wa Libya akanusha madai ya kukutana na maafisa wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79166-waziri_mkuu_wa_libya_akanusha_madai_ya_kukutana_na_maafisa_wa_israel
Kaimu Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Libya amekadhibisha madai kuwa amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 14, 2022 03:05 UTC
  • Waziri Mkuu wa Libya akanusha madai ya kukutana na maafisa wa Israel

Kaimu Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Libya amekadhibisha madai kuwa amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abdul Hamid Dbeibah amekanusha vikali ripoti ya baadhi ya vyombo vya habari kwamba amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Israel katika mji mkuu wa Jordan, Amman.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya mpito ya umoja wa kitaifa ya Libya imesisitiza kuwa: Hilo halijafanyika, na wala halitafanyika katika siku zijazo, kwani msimamo wetu juu ya kadhia ya Palestina uko thabiti na wazi kabisa.

Taarifa hiyo ya serikali ya Libya imekuja baada ya televisheni ya Saudi Arabia ya Alarabiya Alhadath kurusha habari za uvumi kwamba, Dbeibah amekutana mjini Amman na Mkuu wa Shirika la Kijasusi la Utawala wa Kizayuni wa Israel (Mossad).

Maandamano ya kutaka kususiwa Israel

Ripoti hiyo ya upotoshaji ya chombo cha habari cha Riyadh haikueleza tarehe ya kufanyika mkutano huo, lakini inadai kuwa wawili hao walikutana kwa ajili ya kujadili suala la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.

Nchi sita kati ya 22 za Kiarabu ambazo ni Misri, Jordan, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu, Morocco na Sudan zina uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.