Le Point: Tunisia inaporomoka kuelekea kuzimu
Nchi ya Tunisia ambayo miaka 11 iliyopita, ilisifiwa kwa kuwa kinara wa demokrasia kati ya nchi za Kiarabu zilizokumbwa na wimbi la mapinduzi ya wananchi na kupewa hadhi ya kuwa mgeni wa heshima katika mkutano wa G7, sasa inaonekana kufifia na kuorodheshwa kati ya nchi za kifisadi.
Hayo yameandikwa jarida la Ufaransa la Le Point kutokana na ripoti ya kila mwaka ya Kundi la Migogoro ya Kimataifa, ambalo huuainishia Umoja wa Ulaya nchi 10 zilizo katika hatari ya migogoro au kuongezeka kwa ghasia katika kipindi cha mwaka mzima.
Makala hiyo iliyopewa anwani ya: "Tunisia, Nchi Inayoporomoka Kuelekea Kuzimu", imesema orodha ya nchi zinazotajwa kuwa fisadi sasa imeiweka Tunisia kandokando ya majina ya nchi kama Afghanistan ya Taliban na Ukraine iliyozusha mgogoro mkubwa wa kimataifa na kuibua uhofu ya kutokea vita vikubwa kati ya madola yenye silaha za nyuklia duniani. Limeandika kuwa, watafiti wa Kundi la Migogoro ya Kimataifa wamethibitisha rasmi kuporomoka kwa demokrasia changa ya Tunisia.
Gazeti la Le Point limeongeza kuwa, hakujabakia chochote katika mapinduzi ya wananchi wa Tunisia isipokuwa picha yake tu na kwamba kutokuwepo mageuzi kumezusha hali ya kutoaminiana nchini humo.
Gazeti hilo la Ufaransa limesema kuwa, kwa sasa nchi ya Tunisia inaongozwa kwa sheria zilizobuniwa na mtawala wa sasa wa nchi hiyo, Kais Saied mwenyewe na kwamba hali inazidi kuwa mbaya huku nchi ikizongwa na matatizo ya kifedha na kiuchumi.
Katika hatua yake ya karibuni ya kuhodhi madaraka yote ya nchi, Rais Kais Saied wa Tunisia ametangaza habari ya kulivunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama, huku msuguano mkali ukiendelea kushuhudiwa baina yake na mhimili huo wa dola.
Uamuzi huu wa Rais wa Tunisia unaonekana kuwa muendelezo wa hatua anazozichukua kwa ajili ya kudhibiti masuala yote ya nchi.
Miezi kadhaa iiliyopita Rais Kais Saied wa Tunisia alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha akatwaa udhibiti wa masuala yote ya utendaji nchini humo.