Rais wa Tunisia aanzisha Baraza Kuu la Mahakama la muda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80296-rais_wa_tunisia_aanzisha_baraza_kuu_la_mahakama_la_muda
Rais Kasi Saied wa Tunisia ametangaza kuanzisha Baraza Kuu la Idara ya Mahakama la muda baada ya kulivunja lile lililokuwepo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2022 04:21 UTC
  • Rais wa Tunisia aanzisha Baraza Kuu la Mahakama la muda

Rais Kasi Saied wa Tunisia ametangaza kuanzisha Baraza Kuu la Idara ya Mahakama la muda baada ya kulivunja lile lililokuwepo.

Katika taarifa kupitia Twitter na Facebook Jumamosi, Ofisi ya Rais wa Tunisia imetangaza kuundwa baraza hilo la muda siku chache baada ya lile la zamani kuvunjwa.

Taarifa hiyo imesema Rais Saied anasisitiza kuhusu haja ya kuwepo mfumo wenye uadilifu wa sheria ambao unazingatia haki mbele ya sheria huku akisisitiza kuhusu umuhimu wa kuheshimu uhuru wa idara ya mahakama.

Baraza lililovunjwa la mahakama limekaidi amri ya rais ya kulivunja na kusema litaendelea kufanya kazi zake.

Juzi zaidi ya majaji 200 na wanasheria nchini Tunisia walifanya maandamano nje ya jengo la Mahakama Kuu mjini Tunis kupinga tangazo la Rais Kais Saied la kuvunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama ya nchi hiyo. Wakiwa wamevaa nguo zao za kazi, majaji na wanasheria hao wamemtaka Rais Saied aliache kama lilivyo Baraza Kuu la Idara ya Mahakama (CSM) wakionya kwamba hatua yoyote ya kulivunja baraza hilo ni sawa na kukanyaga haki na uhuru wao.

Maandamano Tunisia

Uamuzi wa Kais Saied wa kuvunja Baraza Kuu la Idara ya Mahakama umekuja baada ya kuwakosoa vikali majaji katika miezi ya hivi majuzi. Amekuwa akisema mara kwa mara kwamba hataruhusu kuwepo nchini "serikali ya mahakama" na kwamba idara ya mahakama katika serikali inatosha.

Weledi wa mambo wanasema Kais Saied anakusudia kujirundikia madaraka yote mikononi mwake na pia kuondoa watu, nafasi au taasisi yoyote ambayo inachukuliwa kuwa tishio kwa mamlaka yake. Rais wa Tunisia ameandaa mazingira ya kuwaondoa wapinzani wake wakubwa kupitia vyombo vya mahakama.