Uganda kusitisha ushirikiano wa kijeshi na Korea Kaskazini
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema karibuni hivi nchi yake itasitisha ushirikiano wa kijeshi na kiusalama na Korea Kaskazini.
Jeong Yeon-guk, Msemaji wa Rais wa Korea Kusini, Park Geun-hye amesema kikao kati ya marais hao wawili mjini Kampala kimeafiki kuwa, Uganda itasitisha ushirikiano wake wa kijeshi, kipolisi na kiusalama na Korea Kaskazini. Msemaji huyo wa Rais wa Korea Kusini amesema Rais Museveni ametoa agizo kwa maafisa husika wa serikali yake kutekelezwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoitaka jamii ya kimataifa kusimamisha ushirikiano na Korea Kaskazini ukiwemo ushirikiano katika uga wa usalama. Imearifiwa kuwa, Uganda ni mwenyeji wa maafisa usalama 45 wa Korea Kaskazini, ambao wanatoa mafunzo ya kipolisi na kijeshi kwa askari wa nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika. Jopo la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa karibuni hivi lilisema Korea Kaskazini imekuwa ikiwapa maafisa wa polisi wa Uganda mafunzo ya kutumia bunduki aina ya AK-47 na bastola.
Kwa mujibu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa, serikali ya Pyongyang na jeshi lake hairuhusiwi kuuza, kununua au kutoa mafunzo ya kijeshi kwa nchi nyingine.
Siku chache zilizopita, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilipuuzilia mbali ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa iliyodai kuwa nchi hiyo imekuwa ikipokea silaha kutoka Korea Kaskazini.