Kuongezeka mashambulizi ya utumiaji silaha nchini Msumbiji
Msemaji wa polisi ya Msumbijii amesisitiza kuwa, kushadidi mashambulizi ya utumiaji silaha nchini humo ni jambo linalotia wasiwasi.
Inacio Dina, msemaji wa polisi ya Msumbiji ameongeza kuwa watu wasiopungua 25 wameuliwa na kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wenye mfungamano na chama cha upinzani cha Renamo katika maeneo ya kusini na mashariki mwa nchi hiyo. Ameongeza kuwa hali ya mambo ya Msumbiji hivi sasa ni ya kutia wasiwasi.
Siku kadhaa zilizopita wanamgambo wenye mfungamano na chama cha upinzani cha Renamo walipambana vikali na vikosi vya jeshi la Msumbiji katika jimbo moja magharibi mwa nchi na kusababisha vifo vya wanajeshi 45.
Chama cha upinzani cha Renamo ambacho kwa muda wa miaka 16 kilikuwa moja ya sababu kuu za kutokea vita vya ndani huko Msumbiji kutokana na kuungwa mkono na baadhi ya nchi ajinabi, kwa mara nyingine tena kimetoa vitisho kwa viongozi wa kisiasa wa Msumbiji kuwa kitaanzisha machafuko mapya nchini. Msumbiji imeendelea kubaki nyuma kiustawi kwa kukosa amani na uthabiti wa kisiasa na kiuchumi licha kupita miongo minne tangu nchi hiyo ipate uhuru.