Wasiwasi wa UNHCR kuhusu kutimuliwa Waeritrea nchini Sudan
Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi la UNHCR limesema, lina hofu kubwa na hatua y ahivi karibuni ya kutimuliwa raia wa Eritrea walioko Sudan.
Shirika hilo limesema, takriban Waeritrea 300 walikamatwa Mei 6 kwenye mji wa Dongola, kaskazini mwa Sudan.
Walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kuingia Sudan kwa njia haramu chini ya sheria za kimataifa za uhamiaji na walilazimishwa kurejea nyumbani.
Nora Sturm, msemaji wa UNHCR mjini Geneva amesema, "Sita kati yao walitambuliwa kuwa ni wakimbizi, na wengine hawakuwa wameomba hifadhi lakini ni vigumu kufahamu iwapo walipatiwa fursa ya kufanya hivyo."
UNHCR inasema hiyo si mara ya kwanza kwani kabla ya Mei 22 raia wengine 129 wa Eritrea walikmatwa na kurejeshwa kwa nguvu nchini kwao.
UNHCR imesema kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi, waomba hifadhi au watu wanaohitaji ulinzi ni kinyume cha sheria za Sudan na mkataba wa kimataifa wa wakimbizi wa 1951.