Tunisia yapinga ushiriki wa Israel katika maneva ya Simba wa Afrika 2022
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i85178-tunisia_yapinga_ushiriki_wa_israel_katika_maneva_ya_simba_wa_afrika_2022
Wizara ya Ulinzi ya Tunisia imepinga ushiriki wa jeshi la utawala wa haramu wa Israel katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi "African Lion 2022" (Simba wa Afrika 2022).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 25, 2022 22:39 UTC
  • Tunisia yapinga ushiriki wa Israel katika maneva ya Simba wa Afrika 2022

Wizara ya Ulinzi ya Tunisia imepinga ushiriki wa jeshi la utawala wa haramu wa Israel katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi "African Lion 2022" (Simba wa Afrika 2022).

Wizara ya Ulinzi ya Tunisia ilitangaza katika taarifa yake ya jana Jumamosi kwamba mazoezi ya "Simba wa Afrika 2022" yatafanyika kwa kushirikisha vikosi vya jeshi vya Tunisia na Marekani bila ya kuwepo vikosi vingine.

Katika taarifa hiyo, Tunisia imepinga vikali na kukataa kushirikishwa wanajeshi wa Israel katika mazoezi hayo ya kijeshi kutokana na unyeti wa uhusiano na Algeria.

Algeria inapinga mapatano ya baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel na inaona kuwa utawala huo ni tishio kwa usalama wa mataifa ya Afrika.

Mazoezi ya kijeshi, Tunisia

Algeria pia imepinga hatua ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ya kuupatia utawala haramu wa Israel hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika (AU) ikisema ni kosa makubwa sana.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema hatua ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ilikuwa uamuzi mbaya wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, ambao ulichukuliwa bila ya kushauriana na wanachama wa umoja huo. 

Juhudi hizo za Algeria zilizaa matunda mapema mwaka huu baada ya Umoja wa Afrika (AU) kuusimamisha nafasi ya mwanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo na tayari imeundwa kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika ikiwemo Algeria kushughulikia suala hilo.

Mazoezi ya kijeshi Simba wa Afrika 2022 yanafanyika katika nchi za Ghana, Tunisia, Morocco na Senegal.